CHUMBA HIKI USIFUNGUWE

Karibu mgeni wangu mwenye taadhima na heshima ilotukuka,
Taarifa za ujio wako zilinifanya nikajiandaa vema kwa mapokezi.
hakika nilisafisha nafsi, roho na mwili, niliyaonya matendo yangu dhalimu nikayakemea yasijitokeze kamwe nikiwa nawe.
nilipojua waja niliandika waraka mreefu wa maneno ya vitisho kuziogopesha hisia mbaya zinitumazo kwenye zinaa nikaziambia habii!! zikae mbali nami kamwe zisinisogelee maana ni wewe ndio hupendi machafu yakaribie himaya yako.
niliuonya ulimi uache kuropoka shombo, akili nikaihusia itulie katika kufikiri mema, tumbo nikaliambia liache kudai chakula mchana, ibada nikaziomba zije kuambatana nami ili kukukirimu.
zile spika zangu chumbani zilizozoea kupiga kelele za muziki wa BONGO FLEVA sasa nikazifahamisha kuwa kuna KASWIDA nzuri za kina maherzain.
Kitabu chenye maneno yaloshushwa ndani yako nikakiweka juu mezani, wallah tena naapa ukifika kwangu utakikuta juu tu kinakukaribisha.
Sibishani kwa kupayuka tena. mara zote jirani yangu mlevi akianza kunikorofisha namwambia kwa upole NIPO NAWE MGENI, mgeni mwenye staha, mpole na mwenye hekima.
Namwambia Nimefunga pingu maovu, sina muda wakubishana nae maana kinywa changu sasa kinatema maneno ya toba pekee.
Karibu sana mgeni Duniani ndio nyumba yangu ni ruhusa kutembelea vyumba vyote lakini CHUMBA HIKI USIFUNGUE.
niliposikia waja nikatafuta komeo nakuyafungia yoote matendo yangu maovu ndani ya chumba hiki, ni aibu kusema lakini ukweli ni kwamba ndani ya chumba hiki kuna Masengenyo yangu.
hakika mimi ni msengenyaji, kinywa hiki kinaongoza kwa kuwasema wengine bila wao wenyewe kujua, nimeyafungia hayo ndani ya chumba hiki.
pia ndani ya chumba hiki utakutana na Furushi la Zinaa,ni ukweli kuwa mimi ni Mzinifu na nimeona haya wewe kunikuta mimi na uchafu huo ndio maana nimeamua kufungia furushi hilo ndani ya chumba hiki.
Naomba usikifungue nafsi yangu itanisuta wewe ukiuona uongo niliouficha humo, ni kweli kuwa mimi ni muongo kinywa hiki kimezoea kuzusha hata yasiyo yakweli mradi kufurahisha genge.
Chumba hiki usikifungue kamwe maana ndani yake kuna pesa za haramu, Mavazi yasiyo na heshima,Starehe za dunia, Shirki, usaliti na mengine mengi yasompendeza Mungu.
Nakuomba usikifungue chumba hiki, nisaidie tu kuichukua funguo ya kufuli la chumba hiki kisha ukiondoka ondoka nayo au kama itawezekana mwishoni kabisa ukitaka kuondoka fungua mlango wa chumba hicho kisha fungasha kila kimoja wapo ondoka nacho mie sina shida hata na kimoja kilichomo humo.
Nafurahia zaiwadi zako ulizoniletea IMANI imenijaa, uchamungu nakadhalika, najihisi mwepesi kwa kumtaja Mola wangu kila mara na nikitimiza maagizo yake.
usininyang'anye kamwe neema hizi ulizoniletea maana kesho yangu peponi naiona ikiwa imepambwa na TABASAMU.

Ondoa dhambi zangu, adhabu nisamehewe,
fanya ubaki kwangu, nifaidike na wewe,
niachane na ulimwengu, mgeni wangu nielewe
Naficha aibu zangu, Chumba hiki usifunguwe.


RAMADHAN KAREEM....

Na
Bin Omar Zongo
SIMULIZI ZINAISHI

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »