'tumia vizuri muda huu maana unaweza kukutana na swali gumu baadae halafu ukakosa jibu sababu ya uzembe wa kutolitafuta jibu lake ndani ya muda huu'
Na. Omar Zongo
Muda huu, ndio zawadi pekee ya manufaa iliyo mikononi mwako!.
hebu Vaa uhusika wa marehemu waliopoteza pumzi zao muda mchache uliopita, waonee huruma na utambue kuwa hauna muda wakupoteza na yakupasa uutumie vizuri MUDA HUU.
Muda huu ni kipimo cha kufaulu au kutofaulu huko uendako, kwa ufupi ni kuwa Muda huu ni madini yenye thamani yaliyo kwenye viganja vya mikono yako.
Muda huu utumie sasa kikamilifu, Acha dharau, acha kiburi punguza Hasira na fikiria upya kujenga jumba la furaha nafsini mwako bila kujali nini unapitia na magumu mangapi yanakusonga.
Muda huu acha kuutumia kuvuta sigara sababu unayaumiza mapafu yako na itakugharimu baadae, utumie muda huu kwa kufurahi na yoyote aliye karibu yako, humjui hakujui lakini kama kuna uwezekano wakumsemesha kwanjia ya utani hebu fanya hivyo umjengee kicheko na umuondoe kwenye mawazo ya magumu ayapitiayo maana yanaweza kumpa vidonda vya tumbo.
Usiutumie basi muda huu kwa umbea, uchonganishi na fitina au ukafikira kumteta mtu nakumuongelea mabaya sio vema maana ni muda huu huu ndio ambao linaweza kukuta baya likafanya ujutie kwanini uliutumia muda wako vibaya.
ipe raha nafsi yako usikubali bugdha ya aina yoyote iivamie furaha yako nakuitemea sumu ya simanzi itakayofanya uso wako ukunjamane kuukaribisha uzee ambao nyakati zake bado sanaaa.
Muda huu ni wakupuuza chuki za wanaokuchukia nakuukaribisha upendo wa wanaokupenda
usiishi kwa mazoea muda huu una utofauti na muda mchache uliopita anza sasa kufikiri upya na uone umuhimu wa kuheshimu hisia za mwenzako hasa anayekupenda kwa dhati sababu unapaswa kufahamu kuwa ni wachache sana wenye upendo wa aina hiyo, ukiipuuza hiyo tunu ya kupendwa inaweza kukugharimu miaka yote kuishi bila kuipata tena na hata kama humpendi basi kuwa mwema kwa anayekupenda na ikibidi muheshimu sana.
tumia vizuri muda huu maana unaweza kukutana na swali gumu baadae halafu ukakosa jibu sababu ya uzembe wa kutolitafuta jibu lake ndani ya muda huu.
sio sahihi kuendelea kubeza waswahili na mitazamo yao naamini wana tija na hawajakosea kusema Maisha ni kutafuta sio kutafutana, unaonaje ndani ya muda huu ukaanza kutafuta suluhu ya shida zako na ukaachana na ratiba yako dhaifu ya kuperuzi kujua nani katuma nini mtandaoni au nani ana ugomvi nanani!,
achana na izo habari tambua kuwa ni Muda huu ndio ambao ukienda haurudi tena, basi sawa labda pengine wewe ni mfuasi wa mitandao unaonaje ukaanza kuutumia muda wako kujielimisha hata kwa kuperuzi tu jukwaa la SIMULIZI ZINAISHI kuona utamu wa lugha adhimu ya KISWAHILI, nakuulisha chakula bora ubongo wako.
Fikiri kabla yakutenda, usiruhusu kuulaghai moyo wa mtu kwa uongo jipe ruhusa ya kumuacha haraka sana pale tu unapogundua hauna upendo nae na yupo unayempenda kwa dhati nionavyo mimi kuutumia muda huu kwa kumuumiza mwenzio ni jinai itakayo ihukumu nafsi yako kifungo cha laana huko uendako.
waswahili waloshiba busara na maono ya mbali waliwahi sema Chelewa Chelewa utamkuta mwali si wako, maana yao labda ilikuwa nyengine lakini mimi hapa nitakusihi kuwahi, usichelewe kueleza hisia zako kwa yule umtakae USIOGOPE na wala usijipe sababu zakumwambia muda mwengine, muda mwengine ni siri ya rahmani, wewe wajuaje kama utafika nenda, mueleze, MUDA NDIO HUU!.
utumie vema muda huu kwa kujenga msingi imara wa Amani, pandisha ukuta wa upendo weka lenta ya uaminifu kisha nunua vigae maarufu vya furaha ezeka nyumba yako ipambe kwa rangi ya Upatanishi kisha Chagua maisha ya kuwasaidia wengine, naamini ukiwa hivyo kila siku usiku ukilala ni lazima utaota ndoto nzuuri ya kusaidiwa na wewe.
Yote hayo yatakuwa ni mazao ya kuutumia vema MUDA HUU.
Muda huu usipigane. usigombane wala usimnunie mtu kwa kuhisi amekudhulumu haki yako, amini katika RIZIKI, kila lililo jaala yako hakuna mwenye ubavu wakulinyakua! litakuja tuu kama sio kwa kuletewa basi kwa kushushiwa,
Muda huu usiutumie kwa Kukaa Bure maana Mtembea bure si sawa na Mkaa bure amka kapambane fuata akili yako inapoamini ndipo kwenye ndoto zako, piga hatua zakujiamini maana Mguu wa kutoka Mtume ameuombea.
huu ndio muda ambao mimi nakushukuru wewe maana angalau umeweza kukumbuka sasa thamani ya HUU MUDA kwa kusoma ujumbe huu.
"Ni zaidi ya busara wewe kuwa chanzo cha furaha ya wengine, utaishi kwa amani daima..."
Bin Zongo
SIMULIZI ZINAISHI