NGUVU KUZIMU& UDHAIFU DUNIANI, IZRAEL NAOMBA TUYAJENGE!


BY, Omar A. Zongo

Izrael Mtoa roho nianze kwa kukupa pongezi, hakika Kazi yako umeifanya kwa ufasaha  kuzimu kwapendeza! nami niseme Ahsante kwa kunialika karamu hii ingawa umenisimamisha langoni lakini yumkini naona ndani sina kinyongo, nimeridhika na mwaliko wako!

Izrael wewe ni jemedari bingwa wakuchagua vizuri maana hafla yaendelea ndani lakini navutiwa na jinsi kuzimu ilivyo pambwa naamini ni kazi ya akili yako kuwachukua wapambaji mahiri kutoka duniani!
maandishi yamepambwa kwa umahiri kutambulisha kuwa hii ni NYERERE DAY!
Sina shaka aliyeandika maneno haya kwautashi ulimnyakuwa toka duniania ingawa sijui ni ninani hasa!
jukwaa la kuzimu limepambwa kwa mbadilishano wa sauti za wanamuziki wa kila aina TX MOSHI kwa mziki wa dance akiongoza wanamuziki wenzake wengi kutoka kongo namuona kwa mbaali PAPA WEMBA hakika izrael umeimaliza dunia kama ikitokea karamu kama hii duniani wakali hawa hawapo tena waliopo wanafanya kawaida sanaaaa.

Nasikia kuzimu SIASA yake safi haina ukiritimba fitna na uroho wa madaraka kama ilivyo duniani! hongera izrael kwa kazi nzuri maana ni wewe ndio umeiandaa kuzimu ipate viongozi muktasi! Nawaona kwambaali mababa wa afrika wakipata mvinyo murua huku wakiwa na bashasha yakuijenga kuzimu, Nelson Mandela, Kwame Nkurumah, Julius Nyerere na mashababi kadhaa nawaona wakizungumza lugha moja tu ya UZALENDO wa kuzimu yao maana ni wewe izrael ndio uliwaomba waje huku hakika umetuweza duniani maana falsafa zao zinazungumzwa tu kwa maneno hazifanywi kwa vitendo kamwe na viongozi wa leo wa dunia hii.
Anga la kuzimu lapendeza hakika! harakati zimepatiwa wanaharakati mashuhuri wadunia hii, ni kazi yako Izrael!
kuzimu hakuna ubaguzi warangi tena falsafa za kina Martin Luther king zote zipo huku duniani umetuachia nani??

 Pongezi Izrael kwa kuijenga kuzimu yako nina ombi langu nitaliwasilisha kwako ila acha nikupongeze maana kwa mbaali nausikia mziki wa raggae bila shaka Luckydube na Bob Marley wanafanya yao! hongera maana ladha hizi hazipatikani duniani.

na huu mziki uliomalizika kabla ya raggae duniani tunauita mziki wakufokafoka(HipHop) nimevisikia vionjo vyake kwambaali najua ni hila zako zakuwateka kina Tupack Shakur na BIG, dah! sikujua kama hili ndilo lengo lako hakika kuzimu yapendeza! Michael Jackson
Nasikia sasa hivi anaitwa Mfalme wa Pop kuzimu!

mnakula raha kwa viungo muhimu kutoka duniani naona maigizo yamesheheni waigizaji woote wakali kutoka duniani mpe salamu zangu Blaza Kanumba, nasikitika kuliona chata la THE GREAT likitikisa anga la kuzimu, huku mkichekeshwa na vituko vya sharo, na mkila ladha ya mitindo huru kutoka kwa Albert Mangweir

hakika kama ni kikosi cha timu kocha wewe umeweza kuijenga vema timu yako ya kuzimu ni hatari kila nyanja ipo vema!

Siasa namuona JULIUS NYERERE
Uchumi na Maendeleo namuona STEVE JOBS
Haki za binaadamu safu imekamilika watu imara nawaona wakiongozwa na Martin Luther King!

dah duniani umetuachia nani! mbona kuzimu kwapendeza ilhali mambo yakiwa arijojo duniani.
Nauona ujasiri wakina Mkwawa, uongozi bora wakina Gwangaeto!
nazisikia tenzi na mashairi yakina Shaaban Robert!
Kuzimu umejua kuipendelea kwahila zakuwanyakua watu hawa kutoka duniani.

ahsante kwa kunialika katika karamu hii nimejionea mengi yaliyonijengea tafakuri kichwani mwangu, kabla sijashtuka njozini naomba niwasilishe ombi langu.
naomba tufanye makubaliano Izrael maana duniani hali si shwari! nitaandika hata mkataba wa makubaliano ili kuna watu warejee tena duniani kuweka nguvu namsukumo kwenye masuala muhimu hasa ya kibinaadamu na maendeleo.
siasa imekuwa chungu zaidi ya arovela! anga la dunia lanuka damu, ardhi imeota sugu kwa kuangukiwa na miili ya marehemu wasio na hatia.

mchanga una ladha ya chumvi chumvi itokanayo na damu iliyogandiana na udongo.

vilima hivi sasa haviundwi kwa majabali, lahasha! nasikitika kusema kuwa vilima vingine vinatokana na mrundikano wa maiti walikosa wazikaji.
maeneo ya kuzikia yamejaa pomoni nachelea kusema mwaka huu ukiisha hatutakuwa na pahala pakuzikia.

turejeshee watu kadhaa ambao pengine wanaweza kurejesha mawazo yao tuliyowazika nayo.

Mwambie Baba wa taifa langu Julius Nyerere complimentary aliyokupa unipe nimeipokea na katika hafla hii ya kuzimu NYERERE DAY nimejionea mengi!

naomba ulifanyie kazi ombi langu izrael usiongozwe na tamaa ukanitamani hata mimi kwa huu uandishi uliotukuka! nitagoma kuijenga kuzimu ukinichukua maana ombi langu utakuwa umelipuuzia.
Natamani Isingekuwa ndoto ombi langu ulikubali,


Lakini ajabu unanyanyua mdomo kunijibu nami ndio nashtuka usingizini....

sijakata tamaa naamini nitalala tena na Nitaujulisha ulimwengu...nini umenjibu!


CHIZI MAFANIKIO SEHEMU YA 4

ILIPOISHIA
Bi getrude anasukumwa nakuanguka chini, huku mama yake salim akikimbilia ndani huku analia, tayari mawazo mabaya yalishamuingia kuhusu kifo cha mwanae_

SASA ENDELEA...

Alijisikia vibaya sana kusukumwa namna ile, alijiokota taratibu nakukaa kitako kabla hajaamka nakuanza kumfuata nyuma mama yake Salim.

tayari alishaona dalili mbaya ya chuki ambayo mara zote aliomba isijitokeze katikati yao hasa kuhusu kifo cha Salim.

alijisikia vibaya sana Bi Getrude, aliona namna ambavyo dunia inamgeuka ghafla.

hatua zake ziliishia kwenye mlango wa chumba alichoingia mama yake salim.

ulikuwa umefungwa kwa ndani, alijaribu kugonga mlango nakumsihi afungue lakini maneno aliyojibiwa ndio yalimuumiza zaidi. na alisita hata kuendelea kugonga mlango ule.

" Kamwambie mwanao aje animalize namimi, sioni thamani ya kuendelea kuishi kwakweli mwambie aje aniue kama alivyomuua Salim wangu, alikuwa na makosa gani masikini mwanangu"

kutoka ndani yalisikika maneno haya, ilikuwa ni ghafla mno mama yake salim kubadilika.

 hii ilimshangaza sana Bi Getrude, alinyong'onyea sana kwa maneno yale.

 alitamani hata ardhi ipasuke ajichomeke ndani yake.

licha ya miguu yake kuwa mizito kunyanyuka nakupiga hatua lakini alijitahidi baada yakujishauri kwa muda akaamua aondoke.

maumivu aliyokuwa nayo aliweza kuyahisi mwenyewe tu hakuna ambaye angeweza kuyasimulia, alijiona mwenye hatia, alijiona mkosefu, roho ilimuuma sana.

alianza kuacha viunga vya nyumba ya kina Salim kwa unyonge kabisa, mkononi mwake alikamata zile karatasi alizoandika salim lakini sina uhakika kama alijua amekamata karatasi zile.

ni mwili tu ndio ulikuwa unatembea barabarani lakini akili yake ilikuwa mbali sana kimawazo.

moyoni mwake alitamani Jef apone haraka ili alijue kosa lake, alitamani angegawana maumivu na mwanae huyo lakini aliumia zaidi alipobaini Jef hana uwezo huo wala hang'amui chochote.

akiwa katika wimbi la mawazo hayo ghafla alishtushwa na kelele za watu wakipiga mayowe,

ni hapa ndipo aliposhtuka kijana mmoja akimvuta kwa nguvu kumuondoa barabarani, mapigo ya moyo yalimuenda kwa kasi, mate yalimkauka mdomoni.

almanusura agongwe vibaya na pikipiki iliyokuwa ikijaribu kupenya kwa kulipita gari.

matusi mfululizo yasiyoweza kuandikika hapa yalitoka kinywani mwa dereva yule wa pikipiki.

ni sentesi moja tu ndio angalau naweza kuiweka hapa aliisema yule kijana aliyempakiza mtoto wa shule kwenye pikipiki yake "......kwani ulitumwa ujiuze kwa mkopo......." maneno mengine yaliyoendelea na yaliyoanza hayakuwa yenye heshima na utu hata kidogo kwa mama mtu mzima kama Bi Getrude, lakini ni nani angeweza kumnyamazisha dereva yule wa pikipiki, ambaye alitukana huku akivuta mafuta nakuendelea na safari.

Haikuwa siku njema kabisa kwa Bi Getrude alijiona ni mwenye mkosi mno.

wasiwasi na kihoro vikamfanya akae chini kwa muda kwenye kizimba cha baraza ya watu, kabla ya baadae kujishauri aendelee na safari.

wapo waliomsema kuwa aache mawazo barabarani, na pia wapo waliomfariji nakumtaka ashukuru Mungu kwa kunusurika na ajali ile.

muda alioamua kuondoka katika eneo lile ni muda ambao tayari watu walishaanza kusahau kilichokuwa kinataka kutokea.

kila mmoja sasa aliendelea na shughuli yake.

alibakisha mtaa mmoja tu ili aingie mtaa anaoishi yeye, hatua si chini ya ishirini ndipo sasa akapata pigo jengine ambalo lilimthibitishia kuwa kweli ile haikuwa siku nzuri kwake.

kwa macho yake bila kuhadithiwa na mtu alishuhudia namna ambavyo Jef anagongwa na gari wakati akivuka barabara.

kama kawaida Jef aliongozana na kundi la watoto wakimfuata na walipofika eneo lile la barabara watoto wale walisimama kutazama magari kabla hawajavuka lakini bila kutegemea Jef akawachomoka nakuingia barabarani.

Gari ndogo aina ya brevis iliyo kuwa mwendo kasi ilimvaa bila huruma.

kilichosikika ni milio ya kulalamika iliyotolewa na matairi ya gari kutokana na kusuguliwa kwa nguvu kwenye ardhi ya barabara.

Bi getrude alishindwa kukubali ukweli huu alihisi yupo ndotoni kwa kile alichokishuhudia! nguvu zilianza kumuisha miguuni na baadae machoni mbele yake akaona kiza kinene kikitanda.

karatasi alizokuwa amezishika mkononi zikamtoka bila kupenda na yeye alidondoka chini kama mlevi aliyezidiwa na kileo.

fahamu zikatoweka maungoni mwake....akabaki kimya pale chini! watu kutoka maeneo yote wakaanza kuzunguka eneo lile kushuhudia ajali ya kugongwa kwa Jef.

ni wachache sana ndio walimzunguka Bi Getrude.

Na Omar A. Zongo

INAENDELEA....

NAISIKIA MILUZI

Hekaheka zachachama,kelele huko nyikani
Dawa ya chachu kutema, isibakie  kinywani
Usibaki kutetema, ukavimbiwa tumboni
Nyikani  kwa tanda giza, naisikia miluzi
 
Nyika iliyo salama, hii miluzi ya nini
Kukiepuka kihama, hiyo miluzi acheni
Mioyo yote ya nyama, kutishana kwa fatani
Nyikani  kwa tanda giza, naisikia miluzi

Ebu simameni hima, acheni usubihani
Tulimuomba Karima, atupatie aghani
Tukapewa ilo vema, naomba tuitunzeni
Nyikani  kwa tanda giza, naisikia miluzi

Ukivalia pajama, huku machozi usoni
Utapata tu lawama, nyika ikiwa motoni
Tuende tukichechema, tutunze mali nyikani
Nyikani  kwa tanda giza, naisikia miluzi

Miluzi isiyo mema, yatanda masikioni
Hakuna hata la wema, upoto sio kifani
Tumezaliwa kusema, ila busara pimeni
Nyikani  kwa tanda giza, naisikia miluzi

Mbele tusirudi nyuma, tukachekwa na wageni
Tujengane tu  kwa wema, hekima za duniani
Tukithubutu simama,tutaishia jangwani
Nyikani  kwa tanda giza, naisikia miluzi

Bucha lake ni nyama, sumu huuzwa dukani
Iweje ukasakama, sumu kuuzwa buchani
Fateni tulowatuma, kutuweka furahani
Nyikani  kwa tanda giza, naisikia miluzi


Akili za ukilema, zaweka nyika tabuni
Tujadili kwa heshima, shaka zote za nyoyoni
Tupate jibu la wima, kwa kudura ya Manani
Nyikani  kwa tanda giza, naisikia miluzi


Hii miluzi kikoma, yatakwisha mdomoni
Nawaeleza mapema, yatazameni  ya ndani
Afya bora na uzima, ni jambo zingatieni
Nyikani  kwa tanda giza, naisikia miluzi


Lifikapo la kusoma, someni bila miwani
Mmejaliwa karama, ulimbukeni wa nini
Kujiridhisha mtima, hiyo miluzi acheni
Nyikani  kwa tanda giza, naisikia miluzi

By Fulgence Makayula


KWENDRAAA

Hii ndio nguvu yawaandishi, neno lolote huweza kuwa mada pana na ikajenga mvuto kwa yoyote....

leo ninalo neno hilo lakiburi na jeuri ambalo limeathiriwa kutoka kwenyeneno adhimu lakiswahili linalotamkwa kwenda.

vijana wakileo wajuaji waso na mipaka wenyewe wanatamka kwa dharau na mashushu wakisema kwendraaa....

nifanye nini nami ni nafsi inayoishi leo, nafsi ambayo haiwezi kuepuka kutamka neno hilo kwendraaa...

leo nalitumia nasema kwendraa, toka mbele yangu fisadi wa huba, usiyejua nini maana yamapenzi.

nafsi ikusute suto kuu la kuzodoa matendo yako haramu uliyoyatenda kwangu licha ya upendo wangu imara niliyokukabidhi bure.

nasema kwendraa sina haja nawe popo mtafutaji hata vilo katazwa na Mungu!

natafakari siti ya daladala naona wafanana nayo maana niwewe ndiyo huruhusu kukaliwa na yoyote mradi tu awe na shilingi yakukulipa.

kwendraa mwana kwenda hunifai kwa kulumangia wala kulia nakachumbari.

iweje nguo yako ya ndani iwe busy kuvuka kama walipwa mshahara kwa zoezi hilo.

hivi nani alikwambia kuchezea hovyo miili ya wenzako ni sifa yenye kupendeza eti nani ulimsikia katika dunia hii akivishwa taji la MALAYA bora wa mwaka.

nasema kwendraa maana gharama zakutibu maradhi utakayonipa ni bora nikatazame mechi ya watani wajadi.

iweje sehemu zako nyeti uzishushe thamani na uziondolee ile sifa yake adhimu yakuitwa sehemu za siri.

iweje dharau zakujulikana nje mpaka ndani yako isambae kote mitaani?
eti iweje wewe uwe bingwa wakugeuza mchezo mgumu wenye heshima kuwa dhalili na wakawaida?

kwendraaa wala sitaki tena kwako ibaki kumbukumbu ya kwamba tuliwahi kufahamiana.

ona sasa hata uvae mavazi yastara utembeapo mtaani idadi kubwa yawatu wanakuona upo mtupu. maana ni wao uliwaruhusu wakakufunua nakukufunika kama chungu cha mboga.

mwili wako umegeuka kuwa smartphone unatumika kwa mawasiliano yaso na mipaka.

hivi nani alikwambia heshima yako inajengwa na pesa tu bila kuthamini vile vilivyo nathamani ndani yako.

kwendraa huna haja yakubembelezwa nami hata kama ungali mzuri mithili ya bara la afrika ningalisema kwendraa sababu ya uchafu ulokisiri ndani yako.

unaachaje kuthamini uzuri wa pendo langu eti kisa umasikini ndio nishiriki na wenzangu hapana No nasema kwendraa sikutaki abadani.

shushu hili lina lengo lakuisuta akili yako mbovu inayokuagiza laana yakutumika iwe vazi lako maishani.

narudia tena kwendaa pita hivina usirudi na njia hii maana nitajichukulia sheria mkononi ili Bin Zongo niwe hatiani kwenye ulimwengu wa Huba.

hakikisha unaisoma story hii BIN ZONGO HATIANI NI NZURI


kwendraaaa.........

NAOGOPA

S
auti ya Bwana Said yajirudia kichwani mwangu yanisononesha mno, namsikia akisema "nilikuwa tayari kumuachia pesa na kila nilichokuwa nacho mradi aniache mzima lakini haikuwa hivyo, alinishambulia nakunitoa macho yangu kabla sjapoteza fahamu nakutoelewa kinachoendelea"

sauti yake yakujuta kupita buguruni siku ile bado yanirudia kichwani mwangu dukuduku la uchungu lanikaba, huruma yanikumba lakini zaidi sura mbaya ya dunia naiona machoni mwangu nawaona walimwengu wenye roho mbaya, wakatili mikononi wameshika silaha za ajabu wakiwawinda binaadamu wenzao usiku na mchana.

natazama pakukimbilia sipaoni nabaini kuwa duniani sio mahala salama tena pakuishi, hofu yanitawala huku nikijitajidi kupingana nayo ili niendelee kuwa jasiri lakini naona sura za wakatili zikizidi kuongezeka zote zikinitisha na matendo yao.

 taratiibu naanza kubaini kuwa sina jinsi yanipasa tu niwe mpole nanikiri kuwa NAOGOPA.

naogopa sana tena sana! maana hakuna pakukimbilia wala hakuna wakunitetea binaadamu wenzangu ndio hao baadhi yao wamegeuka wanyama na ambao hawajageuka nao wanaogopa kama ninavyoogopa mimi.

kila mmoja anaomba asikamatwe yeye na kina scopion maana akikamatwa wengine hawataweza kumtetea,
wengine wanajiita migambo, sungusungu wakivaa uhusika wa watetezi wetu lakini ndio hao wakwanza kutenda jinai usiku nakudhulumu hata roho za raia wema mradi wasiamke watupu.

nabaini kuwa binadamu sasa hawataki kumwaga jasho kwa halali wapate pesa zakununua manukato waondoe harufu ya jasho, kwa pamoja wameamua kumwaga damu wapate pesa kisha wanunue manukato waondoe harufu ya damu iliyotapakaa mikononi mwao.
 Naogopa sasa hata kumpeleka mwanangu shuleni maana nako pia si shwari waalimu nao wameingiwa na uscopion mioyoni mwao wanapiga sio tena kwa bakora wanatumia ngumi, mateke, ile sifa nzuri ya ualimu sasa inakaribiwa na uvundo wa ukatili wakutisha Naogopa kwakweli maana ni mie mzazi ndio nijuae uchungu wa mwana.

naogopa sasa hata kutembea barabarani sababu siijui saa wala dakika ambayo wale jamaa watanifikia jamaa ambao huitana Majina kama 'Mchizi' Msela na mengine mengi yaki uwenda wazimu.

naogopa sana maana dunia hii imekuwa afadhali sasa akujie malaika mtoa roho chumbani kwako atakumaliza kwa ukali na ukatili lakini hautafanana na huu ufanywao na binaadamu wanaotafuta pesa bila kujua pesa hizo zilianza kutafutwa miaka mingi na hakuna hata mmoja aliyesema amezipata na akaacha kutafuta.

natafakari hatma yakuogopa kwangu maana ni simu hii ya smartphone ndio inayowaniwa na wakatili, pesa hizi za kuunga unga ndizo zinazohitajika na wahuni,

masikini yamungu wanakosa kujua kuwa moyo wa mtu ni kichaka kilichoficha mengi pengine yule wanayemuadabisha ana shida kuliko wao.

naogopa sana sababu wizi na ukabaji wa siku hizi umebadilika mno, mwanzoni walikuwepo wakija kwako ukiwa mpole wanakuibia tu bila kukuzuru lkn saiv wanakuibia nabado wanaitamani roho yako.

Naogopa mno! imani imevuka ng'ambo imetoweka kimasikhara, nalaumu kwanini haikuniaga mie mnyonge maana nisingeruhusu iniache.

kutokuwepo kwake kunafanya tunapigwa, tunaonewa, tunaishi kwa hofu na woga, nasikia watetezi wetu wapo lkn naogopa sababu hua wanachelewa sana kufika, yaani muda wao wakifika tayari mtu ameshamalizwa.

Naogopa sana sababu wingu la amani limeshatoweka na lile tumaini lakupata neema ya mvua iitwayo Utulivu haipo tena, naogopa sana maana hili dhoruba la jua kali lenye miale yabisi bisi, visu na mapanga linanitishia mno, naishi huku nikihofu siku yangu ikifika nitatolewa macho kama wenzangu, utumbo au nitavunjwa vunjwa nakisha kutupwa barabarani au relini ili nionekane nimekufa kwa kugongwa ikiwa ni matokeo ya matakwa yao binadamu waleo wanaopenda pesa kuliko utu.

Naogopa mno ndio mana siachi kumuita MUNGU mlinzi asiye na shaka, asiyekula rushwa wala kuhadaika na chochote. namuita yeye sababu huadhibu bila upendeleo,
apendalo hufanyika na hana wivu pia ni mwingi wa huruma.

Mungu saidia nafsi za watu wako wema, shusha gharika kwa waovu, jaza Ujasiri na uwajibikaji kwa walioomba kazi zakutulinda raia, watengeneze wawe na huruma na raia wanyonge, wajitoe kwa dhati kutulinda maana hali si shari.

rahisisha maisha ili ugumu usiendelee kubadilisha mioyo yetu, niondolee huu woga maana unatokana na kutokumjua nani ni mwema nani mbaya maana wote bararani nikikutana nao nyuso zao zimepambwa na tasamu.

naogopa mno MUNGU wangu, usiku nikilala nahofia kuhusu ndugu na jamaa wasakatatonge wanaotembea usiku wasije wakazuliwa nakutendewa maovu.

nina woga sana! woga wangu siogopi binadamu NAOGOPA hizi siku za mwisho ambazo zimefika bila hodi na tuyaonayo ndio haswaa tuliyoahidiwa vitabuni ya kwamba tutashuhudia ukatili wakuzidi na dhambi zakumwaga, hakika hizi ni nyakati za mashaka.

ni lazima UKOSE AMANI, ni lazima UOGOPE, uwe na MASHAKA, hakika NAOGOPA!

www.ommyzongo.blogspotcom....