JIKANE SASA

''jikane kwa pigania maneno kama vile anaringa, ana roho mbaya maana  maneno hayo tafsiri yake ni nzuri kwa nafsi yako yaani nikwamba unajiamini na njia zako na unapambana kwa mafanikio yako kwa kushirikiana na wachache ambao utaamini wao wanakustahili, unaendana nao na wana msaada mkubwa wakukufikisha unapoota kufika'' 

Na.
Omar A. Zongo

Waheshimiwa wahenga walisema kuwa utendapo wema, nenda zako kamwe usingoje shukurani.
wakaibuka wengine wakatanabaisha ni busara mkono wakulia ukitoa wakushoto usibaini.
wakaja wengine wakaunga mkono kwa kusema wema wa aina yoyote hauozi.
ahsante waheshimiwa wahenga, nasadiki lakini zaidi naheshimu mawazo yenu yalo busara pomoni.
kilembwe wenu leo naibua hoja ikiwa ni namna nzuri yakuheshimu fikra zangu nakuzithamini maana nimejaribu kuangaza dunia yote hii sikuona wakuweza kuthamini mawazo ya wengine maana ni watu wa dunia hii ndio walio jaaliwa dharau nakujiona wao na watu wao wanaowahusu ndio bora kimawazo.
sijawahi juta kuwapo kwenye dunia hii yenye vichekesho vinavyoumiza, yaani kucheka natamani na kulia pia natamani.
leo nimewaza umuhimu wakujikana, umuhimu wakujikataa, faida zakupingana na baadhi ya maisha ambayo kwa jicho la kawaida tunaita ni ubinaadamu.
leo nimejikuta nikiiona njia bora kabisa yakuishi kwa amani na ushindi wa mafanikio.
leo ndio nimebaini kupitia njia hii kuwa inabidi ifike mahali ujikane na uwakane pia wale unaohisi wanakuhusu.
leo nimebaini kuwa ni dunia hii ndio ambayo hutabasamu na kuwapa zawadi ya mafanikio wale wenye majivuno, maringo, sifa na roho mbaya.
watu hao kwa jicho la kawaida ndio utawaita majina hayo niliyoyatumia mimi lakini kwa jicho la njia hii yakujikana ni watu wenye kujiamini, wenye akili, wanajiheshimu, kujipenda na kuijua thamani yao.
katika dunia hii ukijifanya mwema uko na moyo wakusaidia kila anayekulilia shida, ni dhiki pekee ndio itakustahili nakukuandama pamoja na majuto yakusaidia wasio na fadhila.
ni watu wema pekee katika dunia hii ndio ambao wao hufa wakiwa wamesaidia idadi kubwa ya ndugu na jamaa lakini vizazi vyao huteseka kwa kukosa hata mtu wakumsaidia kikombe kimoja cha maji.
uko wapi ule wema wa wazazi wao? fadhila iko wapi!? hakika naiona njia bora yakujikana utu wako nakujivika utu mwengine ambao utakufanya uzibe masikio kwa wanaojifanya wanakulilia shida nakufumba macho ili usiwaone wanaojifanya wanakujua.
ni njia hiyo pekee itakufanya uishi mbali na wenye mikosi na wanafiki wanaojifanya wema kwako ili kujinufaisha wao huku katika fikra zao wakiwa hawana hata chembe yakurejesha wema uliowatendea.
sio kila mtu anapaswa kuongea nawewe, kukuzoea na kumsaidia anapokulilia msaada,
jikane pigania maneno kama vile anaringa, ana roho mbaya, haya maneno tafsiri yake ni nzuri kwa nafsi yako yaani nikwamba unajiamini na njia zako na unapambana kwa mafanikio yako kwa kushirikiana na wachache ambao utaamini wao wanakustahili, unaendana nao na wana msaada mkubwa wakukufikisha unapoota kufika.
sio kila mmoja unaekutana nae anapaswa kukuzoea wengine ni vikwazo vyakukufanikishia ndoto zako, kupitia wao unaweza kujikuta hufiki uendako masikini ya mungu kumbe ni kwasababu baadhi ya waliozoeana na wewe ni daraja la chini hawajaandikiwa kufika juu hivyo kufika kwako wewe juu kutabaki historia mpaka uwakatae watu hao! huko ndio kujikana.Jikane sasa!
katika hii dunia sio kila mmoja ameandikiwa mafanikio wengine fungu lao ni ufukara tu sababu ya uvivu wao, kutokuwa na malengo, kupenda starehe, pombe au zinaa.
anza sasa kuchagua watu sahihi kwa kuwakataa uliokuwa nao ambao sio sahihi ikibidi achana nao wote tafuta watu wapya, wafanye marafiki.
haimaanishi ujenge uadui maana kumfukuza mtu sio lazima kumwambia toka.
badilika tu kimpango wako, usipite njia zao,simamia mambo yako bila kuwashirikisha, salimiana nao ukikutana nao kisha endelea na hamsini zako.
amini usiamini watakuelewa tu na wala usijali jiamini na maamuzi yako.
kujikana ni swala gumu maana litakuachanisha hata na baadhi yandugu zako kama sio wote, mpenzi wako na hata rafiki yako wakaribu.
kujikana pia kutafanya hata usiwe mcheshi tena kwa wale waliokuwa wakikusifu mcheshi, utakuwa mchoyo, mbinafsi lakini ni sahihi kuonekana hivyo kwa watu ambao sio sahihi maishani mwako.
wakatae na hakikisha wanajua kuwa umewakataa,
sio ngumu ni rahisi sana hasa ukitafakari nakujua kuwa katika maisha yako nawewe kuna watu walikukataa na wakaishi kivyao, ukawatafsiri vibaya kuwa wanaringa na wanaroho mbaya.
hapana sio hivyo huo ndio ukweli wa maisha
tafsiri ya mtu kuona hakujali, anakuchulia poa nakukuona wakawaida ni kwamba anakuona haumstahili katika maisha yake.
mwenye makosa ni wewe ambaye unahangaika huku na kule kulalamika eti fulani anajisikia, anaringa au sijui amebadilika.
kwa upande wa jamaa yupo sahihi maana ni yeye ndiye ambaye aliamua kuchagua maisha yake nakujipa thamani nakujiona kuwa wewe haumstahili kuzoeana nae.
hii ndio tafsiri, na ibaki kuwa fundisho kwako kuwa nawe unapaswa kuyapa thamani maisha yako na malengo yako kwa kuchagua watu wanaokustahili kuwa nao.
furaha nzuri ni ile unayoijenga mwenyewe kisha ikakufurahisha ni watu wanaotegemea wapate furaha za wengine pekee ndio ambao husongwa na mauimivu daima.
jikane sasa, jikatae kabisa maana kufanya hivi ndio kuyapa thamani malengo yako, nafsi yako na wengine wengi watakuheshimu huku wachache wakikulaumu lkn usijali maana Hata watu wema walilaumiwa sana katika maisha yao.
Na.
 BIN.ZONGO

MTU NA MTUWE; SEHEMU YA 2

"Zawadi nzuri ambayo nipo nayo na nitakuwa nayo daima ni talanta ya uandishi niliyojaaliwa na Mungu, nalazimika kukuzawadia simulizi hii nzuri ya Mapenzi katika msimu huu wa Mahusiano mema kwa wapendanao, msimu wa valentine day, NI KISA CHAKUBUNI AMBACHO NIMEJITAHIDI KUKIMEGA KATIKA SIMULIZI YANGU NZIMA IITWAYO MTU NA MTUWE, NIMEWEZA KUMEGA BAADHI YA VIPANDE NIKAPATA SEHEMU YA KWANZA NA YAPILI.....SONGA NAYO SEHEMU YA PILI YA MTU NA MTUWE''

Na. OMAR A. ZONGO

Ulikuwa ni usiku wa maajabu kwangu, usiku wa vituko na nyingi tashtiti za mapenzi.
usiku wakuamkia SIKU YA WAPENDANAO, nikatika usiku huo ndio ambapo taarifa niliyoisikia kwenye kituo cha luninga cha CNN niliamini kuwa ina ukweli
sasa wazi nilijionea hali ya mambo, nikweli siku ya wapendanao ya mwaka huu ilikuwa ya ajabu. KILA MTU ATAMFUATA ANAYEMPENDA KWA DHATI.
tayari Victoria alinifata mimi huku mimi nikimsihi Jamila wangu atulie wakati Jamila mwenyewe alishamkumbuka X wake aitwae Edy.
tayari saa sita na dakika zake kadhaa zilitimu, tayari siku ya wapendanao ilifika.
nilibaki nimeduwaa nikimtazama Victoria kwa mshangao, mimi na yeye tulishatengana kitambo tu na sababu ya kutengana nae ni kutokuwa na mapenzi ya dhati nayeye nilihisi nikiendelea nae penzini nitamuumiza tu.
"siwezi ishi bila wewe" alisema Vicky "nakupenda kutoka ndani ya moyo wangu, usinikatae tafadhali" alimaliza kuongea kwa hisia kali.
nilijikuta nachanganyikiwa, wakati sijui nini nimjibu ghafla mlango ukafunguliwa kwa nguvu akaingia jamaa flani sikumjua jina lake.
jamaa bila hata salamu akapiga magoti mbele yangu huku akilia kama mtoto. " tafadhali sana brother naomba uniachie Vicky wangu, nampenda sana yeye ndio kila kitu kwangu."
hee!! nini iki kinaendelea mbele yangu kabla sijamjibu jamaa simu yangu ikaanza kuita mfukoni, niliitazama nikaona ni rafiki angu Bonge ananipigia, nilijishauri kwa sekunde kadhaa nipokee au nisipokee lakini mwisho nikaona nipokee! Bonge alikuwa analia kama mtoto!
"dullah Jeni hanitaki, jeni ameniacha hii leo kamfata James....Dullah nisaidie kumrudisha Jeni wangu ni wewe ndio unajua kwa jinsi gani nampenda Jeni wangu....." aliongea kwa sauti ya majonzi Rafiki angu Bonge, nilistaajabishwa sana na habari ile....James alikuwa ni rafiki yetu na walikuwa marafiki pia na mpenzi wa Bonge aitwae Jeni, sakata lilichukua sura mpya. sasa nikaamini ukweli wa Taarifa niliyoisikia asubuhi.
Sijui ni mtandao au nini lakini kabla sijamjibu Bonge ghafla simu yake ikakata.
kitu kimoja nikaja kugundua kuwa mtandao kwa siku ile ulikuwa wa shida sana, huwezi amini kila mtu siku ile alikuwa anamtafuta wake wamoyoni anayempenda kweli.
akili yangu iliporejea mule ndani nilibaini Jamila ameshatoka mule ndani, nikajiuliza ameenda wapi, lakini jibu likaja kuwa ameenda kumtafuta Edy.
ndani nilibaki na Vicky na yule jamaa aliyenipigia magoti kama mtoto mdogo. dah mapenzi kweli nikitunguu kikikuingia barabara jichoni lazima utokwe na chozi, jamaa bado alikuwa akilalama namimi eti nimuachie Vicky wake.
ugomvi ukaibuka Vicky akaanza kumshutumu jamaa kuwa anamuharibia penzi lake nakwamba hamtaki anataka kuwa namimi
vicky hakuwa hata na chembe ya huruma kwa kijana wa watu.
kusema kweli mimi akili yangu yote ikahama katika ile hali inakuaje lakini ghafla wakati nawaza chakufanya kubaini undani wa ile hali kwanini kila mtu anamfata ampendae akili ikanituma niingie ndani.
nikakimbilia huko, moja kwamoja nikaiendea album yangu, kuna picha yangu ya kitambo kidogo nilipiga na mpenz wangu wakwanza anaitwa Semeni, nilijikuta naitandika bakora za mabusu picha ile nilijikuta namkumbuka sana semeni, machozi yakanitoka nilipobaini siwezi kumuona tena.
masikini semeni alishafariki miaka sita iliyopita kwa ajali ya gari. nilikuwa nampenda sana binti yule, bila kujali kuwa ni usiku nilijikuta natamani kuelekea makaburini kwenda kwenye kaburi la Semeni nakumueleza kwa jinsi gani nampenda.
nilijikuta nalia kwa sauti ya kwikwi huku nikitoka nakuwaacha Vicky na Jamaa ake niliwaonya wasinifuate. Vicky alilia sana huku jamaa ake akiendelea kumbembeleza.
nilifika kwenye gari langu nakuanza safari yakuelekea kinondoni makaburini mahali ambapo semeni mpenzi wangu alipumzishwa.
nilistaajabu sana nilipofika makaburini! watu walikuwa wengi bila kujali kuwa ni usiku, kila mmoja alikuwa kwenye kaburi la ampendae akilia kwa nguvu na kwa uchungu. mimi sikujali sana nikasogea kwenye kaburi la semeni ajabu nikamkuta jamaa mwengine akilia huku akimuita semeni.
"nilikupenda sana semeni, sikuwahi kukwambia enzi za uhai wako, leo hii nimejisikia kukueleza ukweli wangu!!!." alilalama hivi jamaa yule kwakweli licha ya kwamba Semeni alikuwa ameshafariki lakini niliingiwa na wivu wa ajabu.
nikamsogelea jamaa nakumvuta kwa nguvu! loh alikuwa ni kaka angu watumbo moja yeye aliitwa Ommy!.
ilikuwa ni siku ya wapendanao ya historia, siku iliyoandikwa kwa mfululizo wake kwenye kitabu hiki kizuuri kilichokuwa mikononi mwangu! aliyeniondoa katika wimbi la mawazo ya visa vizuuri vya mapenzi vilivyomo katika kitabu kile ni Rafiki angu Jafety, alianza kimasikhara kulalama tumbo linamuuma lakini sasa akawa anaonekana maumivu yamemzidi! nilikifunika kitabu kile kiitwacho MTU NA MTUWE.
nikamsogelea Jafety kumuuliza hali yake.!
kwakweli utamu wa simulizi ya ile uliendelea kubaki kichwani mwangu hadi nilipokuwa njiani kumpeleka Rafiki angu hospitali.
nilitamani sana kujua siku hiyo ya valentine iliishaje nikweli kila mtu alibaki na mtu wake ampendae na je nikweli duniani watu wanaishi na watu ambao hawawapendi kwa dhati.
nilijuliza maswali mengi sana huku nikitaka kujua mustakabali wa wale ambao waliowapenda kwa dhati wameshatangulia mbele ya haki.
Nilijikuta navutiwa sana na utamu wa kitabu kile MTU NA MTUWE mtunzi wake ni OMAR ZONGO....sema niliahidi nafsi yangu lazima nikamalizie story ile.
Sorry mimi sijawatajia jina langu naitwa FARAJA, Jafety ni rafiki angu amenitembelea leo kwangu ndio ghafla amekamatwa na maradhi ya tumbo acha nimuwahishe hospitali.

MWISHO
Na.
BIN ZONGO
ommyzongo.blogspot.com
SIMULIZI ZINAISHI...

MTU NA MTUWE; SEHEMU YA 1

"Zawadi nzuri ambayo nipo nayo na nitakuwa nayo daima ni talanta ya uandishi niliyojaaliwa na Mungu, nalazimika kukuzawadia simulizi hii nzuri ya Mapenzi katika msimu huu wa Mahusiano mema kwa wapendanao, msimu wa valentine day, NI KISA CHAKUBUNI AMBACHO NIMEJITAHIDI KUKIMEGA KATIKA SIMULIZI YANGU NZIMA IITWAYO MTU NA MTUWE, NIMEWEZA KUMEGA BAADHI YA VIPANDE NIKAPATA SEHEMU YA KWANZA NA YAPILI.....SONGA NAYO''

NA. OMAR A. ZONGO

Mie na valentine wangu tulikuwa nayo desturi yakutazama habari za ulimwengu kupitia Shirika la utangazaji la CNN.
hii ilikuwa ni asubuhi mishale ya saa ni saa kumi na mbili.
miongoni mwa habari zilizonishangaza ni ile iliyosema kuwa eti Siku ya wapendanao kwa mwaka huu itaadhimishwa kwa maajabu makuu.
Habari hii ilieleza kuwa kutokana na dhulma na kuibiana wapenzi
mwaka huu mioyo ya watu imeamua kufunguka na kueleza kwa vitendo ni yupi anapendwa kwa dhati.
habari ile ilisema kuwa uongo wote katika mapenzi utakoma siku ya tarehe 14 mwezi febr.
Mpenzi wangu alinitazama huku uso wake ukionekana wazi una mastaajabio na maswali mengi kuhusu taarifa ile.
"inawezekana vipi???" akajikuta akihoji hivi.
sorry sijawatajia jina mpenzi wangu huyu anaitwa Jamila.
miongoni mwa wanawake warembo waliofanikiwa kuuteka nyara moyo wangu, mpole na mjuzi wa mambo hasa awapo kwenye ule uwanja wafundi seremala.
nilikosa chakumjibu Jamila wangu kichwani mwenyewe nikabaki nikiitafakari taarifa ile, yaani kama ingekuwa imetangazwa kwenye chombo cha habari cha kawaida ningehisi ni mbinu yakuteka tu wasikilizaji katika siku hiyo ya wapendanao.
nilijaribu kufuatilia media nyengine hakukuwa na taarifa ile mpaka nikahisi labda nimejichanganya mwenyewe kutokana na CNN wanazungunza kiingereza huenda wakawa wameniacha, Lugha Gongana.
tulijadili kidogo na hubby mwisho tukaangukia kwenye utani.
"hivi kama ikiwa nikweli itakuaje swthert maana kila mmoja ataangukia kwa ampendae mnh hivi wewe utabaki namimi kweli???" nilijkuta nahoji kuhusu tafakuri yangu ndogo iliyokuwa ikikatiza kichwani mwangu.
jamila alicheka kisha akanijibu "ah niende wapi mie nishazama kwako" alijibu hivi Jamila, jibu ambalo lilinifariji sana.
asubuhi ile tukaagana vizuri na Jamila mpenzi wangu nikaelekea kazini, wakati niko kwenye gari langu naendesha huku nasikiza redio mojawapo maarufu nchini tanzania ghafla nikaanza kuwasikia watangazaji wakiulizana kuhusu taarifa ile niliyoisikia asubuhi
umakini wakusikiliza ukaongezeka, hata watangazaji wenyewe walikuwa hawaamini kuhusu taarifa ile huku wengi wakihoji itawezekana vipi.
kwa mujibu wa CNN walieleza kuwa ule ni utafiti uliofanywa na wanasaikolojia wa HUBA kutoka katika ulimwengu wa mapenzi ambao haujulikani upo upande gani mwa dunia hii.
huwezi amini
mitandaoni mada ikawa ndio hiyo, jumbe fupi za kuchekesha ziliundwa fasta watu wakitumiana.
mojawapo ni hii
'pale valentine hii unapojikuta unamuacha uliye nae nakuelekea mirembe maana umpendae yupo huko'
meseji za namna hii zilisambaa kote huku kila mmoja akielekezea hisia zake kuhusu suala lile.
wengi walikuwa kama mimi ilikuwa ni ngumu kuamini kama inawezekana ikawa hivyo.
ilikuwa ni baada ya siku ile ndio siku ya wapendanao ifike wengi walisema haiwezekani huku wakiisubiri kwa hamu ile siku ifike.
nakumbuka siku ile nilifanya kazi mpaka saa mbili usiku nikarejea nyumbani.
wakati naendesha gari mawazo yangu yote yalikuwa kwa Jamila Mpenzi wangu, niliwaza nakuwazua nikitu gani nifanye vilentine hii kumfurahusha hubby wangu.
kutokana na foleni barabarani siku ile nilifika nyumbani saa nne kasoro usiku, kwakweli nilichokikuta siikutaka kuamini.
Jamila alikuwa amepoteza kabisa furaha yake ya siku zote, nilijikuta nambembeleza sana aseme tatizo.
Baadae akawa tayari kunieleza, Loh! nilijuta kumbembeleza.
ni kitambo sana hajamgusia mpenzi wake wa kwanza aliyeitwa Edi, jamaa alimuumizaga sana Jamila enzi wapo wote.
mpaka nampata mimi Jamila bado alikuwa anampenda sana Edi, alikuwa hawezi kupitisha muda flani bila kumtaja mshkaji.
ilikuwa inaniumiza sana hali ile lakini sikuchoka sababu nilikuwa nampenda sana Jamila, nashukuru baada ya muda akanizoea na tukaishi wote kwa furaha na mipango ya harusi yetu ilikuwa inakaribia.
nilishangaa sana kauli zake za siku ile alidiriki kusema kuwa anajilazimisha tu kunipenda lkn moyo wake wote bado upo kwa Edi.
Ulikuwa ni ukweli mithili ya msumari wa moto kwenye mtima wangu.
usoni mwake Jamila alionekana akimaanisha anachosema.
wakati nimepigwa na bumbuwazi ghafla mlangoni kuna mtu alikuwa akibisha hodi.
mimi nilienda kufungua, duh! alikuwa ni Victoria, mpenzi wangu nilieachana nae huyu binti alikuwa ananipenda sana! niliachana nae tu sababu moyo wangu ulizama zaidi kwa Jamila.
Victoria alikuwa ametota machozi! aliniambia amefuata penzi lake.
HABARI ILE YA ASUBUHI ILIKUWA INA UKWELI MBONA MAMBO HAYA SIYAELEWI! NILITAZAMA SAA ZILIBAKI DAKIKA CHACHE TU IFIKE SAA SITA SIKU IBADILIKE IWE SIKU YA VALENTINE DAY!
sorry sijawatajia jina langu Mimi Naitwa Dulla
balaa hili linamuendelezo wake sehemu ya pili USIKOSE KUFUATILIA.
blog hii kwa simulizi nzuri za kila aina
ommyzongo.blogspotcom
SIMULIZI ZINAISHI!
Na,
BIN ZONGO

USIMUAMINI

Bora tu kuwa muwazi nakupinga uongo wakumpamba kwa maneno mazuri yanayomfanya umuone mwema!

fungu utakaloniweka utajua mwenyewe ila mimi nakuambia ukweli USIMUAMINI! ndio, usimuamini kwa lolote asemalo labda akuthibitishie kwa vitendo nawewe ujiridhishe kweli ametenda yeye maana uongo upo hata kwenye utendaji!

tangu kuzaliwa kwake jicho hili limeona mengi nakujifunza vingi pia, moja ya fundisho ndilo hilo nakuasa nalo KAMWE USIMUAMINI!

nimuongo, mzandiki na mjanja kupindukia ukiyaamini majibu yake hakika utapotea, suala la msingi ni moja tu usimuamini!

kama huniamini hebu Tafuta vitabu vyooote vya mapenzi na usome hulka za wapendanao nina uhakika hakuna hata mmoja aliyewahi jibu kuwa sio muaminifu pindi alipoulizwa na mwanza wake kama ni muaminifu!

uhakika ninao kila mmoja hujibu kuwa yeye ni muaminifu tena wa kiwango cha juu tena ubaya zaidi huweza hata kupitisha kidole chake shingoni akiapa kwa jina la MUNGU wake kuwa yeye ni muaminifu wakati ukweli sio huo! hata HOFU ya MUNGU hana aisee USIMUAMINI!

ukiutafuta ukweli unaweza kubaini kuwa yeye ni bingwa wakudanganya, moyo wake umezingirwa na wapenzi lukuki, na kila mmoja amempa nafasi kubwa yakuutalii mwili wake! Yani sijui hata kwanini siku hizi uongo ndio pambio la mapenzi nina uhakika kama ingekuwa sio hivyo walau asingeongopa kuwa yeye ni muaminifu wakati ni zaidi ya mzinifu, bingwa wakucheza mechi za nje!

usimuamini sababu hakuna aliye mkweli katika mahusiano nionavyo mimi kila mmoja sasa hivi ana tamaa ya kile anachokikosa kwa mpenzi wake.

usimuamini kabisa maana ukitafuta kote ulimwenguni utagundua kuwa ni wachache mno waliopata ujasiri wakujitangaza kuwa wameathirika na UKIMWI, wengi wanavinjari nawadudu huku wakionesha ubukheri wa afya kumbe ukweli damu zao ni HATARI TUPU na ibilisi wa roho mbaya anawaongoza kusambaza bila huruma, pengine uliye nae sio mmoja wao lkn unajuaje kama amekutana na watu wa aina hii akawaamini nakujizolea maradhi! tafadhali ndugu yangu USIMUAMINI maana hata yeye pengine hajijui.

kutokumuamini mtu sio dhambi wala jinai nijuavyo mimi ni njia nzuri ya kujihami na maovu, majuto pamoja na athari nyengine zitokanazo na walimwengu walioficha mengi mioyoni mwao.

Usimuamini kabisa maana hata wewe sidhani kama ulishawahi kusema kwa mpenzi wako kuwa ulimsaliti au unamsaliti na rafiki yake au mtu yoyote wa nje, nijuavyo mie ni lazima unampamba kwa maneno mazuri ya uongo ukijinasibu kuwa wewe ni mtulivu, muaminifu na kamwe hutakuja kumuumiza! ndio huu ndio uongo uliopo lkn tukisimamia ukweli Usaliti nimkubwa miongoni mwetu sasa kuna haja gani yakumuamini uliye nae wakati wewe mwenyewe ni shahidi wanafsi yako kuwa unapiga matek two mengi kwa siri!.

nasema hivii...Hakuna kuaminiana kama vipi!.

kwa mfano mawasiliano yangekuwa kama yafuatayo duniani labda pengine ningefuta kauli yangu hii ya USIMUAMINI.

"mpenzi wangu wakati umesafiri nimekusaliti mara 4 na watu tofauti tofauti na mwisho wakukusaliti nj jana usiku nilitoka na best ako, so plz baby kabla hatujamet naomba tusubiri kwanza tukacheki afya! nisamehe sana mpenzi wangu kwa ukweli huu!!!"

labda haya yangekuwa ni maneno yakawaida kwa wapenzi ningeshawishika kukwambia MUAMINI lakini huo ndio ukweli unaofichwa na UONGO unaowekwa wazi ni huu

"Sijapata siku nyingi sana mpenzi yaani tangu ulivyosafiri nimevumilia, nafurahi umerudi naamini leo nitaburudika nawe, nakupenda sana"

AFANALEKI!!! Kuna haja gani yakuaminiana, eti???? usimuamini aisee!

hio ndio hali ya mambo duniani ilivyo na nitaendelea kupata dhambi kukufahamisha kitu ambacho unachokijua, kwa sasa acha nikwambie chakufanya, nalikaribia sikio lako nakunong'oneza kimbea...... USIMUAMINI!

jipende sana na uipende afya yako! kabla hujampa mwili wako mtu mtathimini kwamuda na kisha nenda ukapime nae! wakati mnaenda pia USIMUAMINI maana anaweza kumuhonga Dokta, kuwa makini.

Rudia nae kupima mara kadhaa sehemu tofauti tofauti na hata kama yuko salama usimpe kwanza mgusie suala la ndoa mradi tu aone kizuizi asikuchukulie poah! naamini ukimzungusha hivyo miezi mitatu itafika nenda mkarudie tena kupima kumbuka haya yote nikabla hujampa, ukimpa tu ujue umeshaweka rehani roho yako haikisha mnapima mara nyingi zaidi kama yuko salama ANZA SASA KUMFIKIRIA!

Sitakwambia kamwe umpe akitakacho maana mimi mwenzio imani yangu inaniambia ZINAA HAIFAI!

"usimuamini mtu ukamuudhi MUNGU wako, imani yako itakuponza, nakusihi sana ndugu yangu USIMUAMINI!"

MUDA HUU


'tumia vizuri muda huu maana unaweza kukutana na swali gumu baadae halafu ukakosa jibu sababu ya uzembe wa kutolitafuta jibu lake ndani ya muda huu'

Na. Omar Zongo


Muda huu, ndio zawadi pekee ya manufaa iliyo mikononi mwako!.

hebu Vaa uhusika wa marehemu waliopoteza pumzi zao muda mchache uliopita, waonee huruma na utambue kuwa hauna muda wakupoteza na yakupasa uutumie vizuri MUDA HUU.

Muda huu ni kipimo cha kufaulu au kutofaulu huko uendako, kwa ufupi ni kuwa Muda huu ni madini yenye thamani yaliyo kwenye viganja vya mikono yako.

Muda huu utumie sasa kikamilifu, Acha dharau, acha kiburi punguza Hasira na fikiria upya kujenga jumba la furaha nafsini mwako bila kujali nini unapitia na magumu mangapi yanakusonga.

Muda huu acha kuutumia kuvuta sigara sababu unayaumiza mapafu yako na itakugharimu baadae, utumie muda huu kwa kufurahi na yoyote aliye karibu yako, humjui hakujui lakini kama kuna uwezekano wakumsemesha kwanjia ya utani hebu fanya hivyo umjengee kicheko na umuondoe kwenye mawazo ya magumu ayapitiayo maana yanaweza kumpa vidonda vya tumbo.

Usiutumie basi muda huu kwa umbea, uchonganishi na fitina au ukafikira kumteta mtu nakumuongelea mabaya sio vema maana ni muda huu huu ndio ambao linaweza kukuta baya likafanya ujutie kwanini uliutumia muda wako vibaya.

ipe raha nafsi yako usikubali bugdha ya aina yoyote iivamie furaha yako nakuitemea sumu ya simanzi itakayofanya uso wako ukunjamane kuukaribisha uzee ambao nyakati zake bado sanaaa.

Muda huu ni wakupuuza chuki za wanaokuchukia nakuukaribisha upendo wa wanaokupenda

usiishi kwa mazoea muda huu una utofauti na muda mchache uliopita anza sasa kufikiri upya na uone umuhimu wa kuheshimu hisia za mwenzako hasa anayekupenda kwa dhati sababu unapaswa kufahamu kuwa ni wachache sana wenye upendo wa aina hiyo, ukiipuuza hiyo tunu ya kupendwa inaweza kukugharimu miaka yote kuishi bila kuipata tena na hata kama humpendi basi kuwa mwema kwa anayekupenda na ikibidi muheshimu sana.

tumia vizuri muda huu maana unaweza kukutana na swali gumu baadae halafu ukakosa jibu sababu ya uzembe wa kutolitafuta jibu lake ndani ya muda huu.

sio sahihi kuendelea kubeza waswahili na mitazamo yao naamini wana tija na hawajakosea kusema Maisha ni kutafuta sio kutafutana, unaonaje ndani ya muda huu ukaanza kutafuta suluhu ya shida zako na ukaachana na ratiba yako dhaifu ya kuperuzi kujua nani katuma nini mtandaoni au nani ana ugomvi nanani!,

 achana na izo habari tambua kuwa ni Muda huu ndio ambao ukienda haurudi tena, basi sawa labda pengine wewe ni mfuasi wa mitandao unaonaje ukaanza kuutumia muda wako kujielimisha hata kwa kuperuzi tu jukwaa la SIMULIZI ZINAISHI kuona utamu wa lugha adhimu ya KISWAHILI, nakuulisha chakula bora ubongo wako.

Fikiri kabla yakutenda, usiruhusu kuulaghai moyo wa mtu kwa uongo jipe ruhusa ya kumuacha haraka sana pale tu unapogundua hauna upendo nae na yupo unayempenda kwa dhati nionavyo mimi kuutumia muda huu kwa kumuumiza mwenzio ni jinai itakayo ihukumu nafsi yako kifungo cha laana huko uendako.

waswahili waloshiba busara na maono ya mbali waliwahi sema Chelewa Chelewa utamkuta mwali si wako, maana yao labda ilikuwa nyengine lakini mimi hapa nitakusihi kuwahi, usichelewe kueleza hisia zako kwa yule umtakae USIOGOPE na wala usijipe sababu zakumwambia muda mwengine, muda mwengine ni siri ya rahmani, wewe wajuaje kama utafika nenda, mueleze, MUDA NDIO HUU!.

utumie vema muda huu kwa kujenga msingi imara wa Amani, pandisha ukuta wa upendo weka lenta ya uaminifu kisha nunua vigae maarufu vya furaha ezeka nyumba yako ipambe kwa rangi ya Upatanishi kisha Chagua maisha ya kuwasaidia wengine, naamini ukiwa hivyo kila siku usiku ukilala ni lazima utaota ndoto nzuuri ya kusaidiwa na wewe.
Yote hayo yatakuwa ni mazao ya kuutumia vema MUDA HUU.

Muda huu usipigane. usigombane wala usimnunie mtu kwa kuhisi amekudhulumu haki yako, amini katika RIZIKI, kila lililo jaala yako hakuna mwenye ubavu wakulinyakua! litakuja tuu kama sio kwa kuletewa basi kwa kushushiwa,

Muda huu usiutumie kwa Kukaa Bure maana Mtembea bure si sawa na Mkaa bure amka kapambane fuata akili yako inapoamini ndipo kwenye ndoto zako, piga hatua zakujiamini maana Mguu wa kutoka Mtume ameuombea.

huu ndio muda ambao mimi nakushukuru wewe maana angalau umeweza kukumbuka sasa thamani ya HUU MUDA kwa kusoma ujumbe huu.

"Ni zaidi ya busara wewe kuwa chanzo cha furaha ya wengine, utaishi kwa amani daima..."

Bin Zongo
SIMULIZI ZINAISHI