Kuanzisha mahusiano ya mapenzi sio dhambi wala jambo baya katika akili ya yeyote aliye timamu.
Lakini ubaya unakuja jitokeza pale ambapo mnashindwana na kushindwa kuamini kama mmeshindwana hivyo kubaki mnavumiliana, mkikondeshana, kudharauliana, kutukanana, kupigana na wakati mwengine hata kuuana.
Jifunze leo hapa kumuacha aende zake, kuitambua,kuiheshimu na kuitumia vizuri siku.
Siku ya kuachana.
Na.
Omar zongo.
Hakikisha muda wa kuachana ukifika unafanya hima muachane.
Using'ang'anie bidhaa ambayo imefika tamati Yake ya matumizi.
Hiyo tayari ni sumu kukuua si ajabu!
Muda wa kuachana una dalili na upo dhahiri.
Ukiona tu mambo yamebadilika, upendo umechujuka, taa imezimika, nakusihi ondoka.
Hakuna Tena zile 'baby' na 'sweetheart' unaitwa kwa jina lako, au 'Apple' na 'Chocolate' ujue ndio mwisho wako.
Kitendo cha 'text' kupungua, zile 'I miss you' kupotea na hakuna kujishtukia ujue muda umewadia.
Muda wa kuchokana una nyingi tashtiti kwanza kugombana, pili kuchuniana tatu kudharauliana na mwisho kutukanana.
Isifike kupigana haraka Sana fanya hima, ni Bora ya kuachana kuliko kuumizana.
Ulipomuona mara ya kwanza alikuvutia, ukajiambia yeye ndiye ule ubavu wako uliomegwa akaumbwa, ukatabasamu ulipomtazama, ukamwambia maneno yote mazuri.
Ukatoa maneno matamu katoka kwenye wimbo ulio bora wa Suleiman, ukamsifia kwa sifa zote, ukamridhia kwa moyo wote na ukamuahidi ahadi zote.
ziko wapi zile siku?, uko wapi wema wako?, yako wapi maneno yako, matendo yako, furaha yako na.... ya mwenzako?
Leo hii kawa mjinga, mpumbavu, havutii, hapendezi na anakera ukimuona!!
Mabadiliko sio mwiko, hutokea na ni kawaida hivyo usiumie unapochokwa au kuchoka.
Ni kosa kulazimisha hasa muda ukishafika, utajitia mashaka na homa Kali ya simanzi.
Tambua Hakuumbwa peke Yake, muache aende zake, yashike mazuri Yake, sahau ubaya wake.
Haukupoteza muda, umejifunza kuwa nae, Kuna Elimu kubwa kaitumie kwengine.
Mwengine kwa ajili yako yupo mahali katulia, kumng'ang'ania yeye ni kupoteza bahati, kumsubirisha wasahihi 'asisogee karibu yako.
Mahusiano wakati mwengine ni kama vile chakula kizuri ukipendacho, kikiwa pale mezani kinapendezea macho.
Lakini ukisha kula, hugeuka matapishi na baadaye kinyesi kinachoumiza tumbo.
Ukishaenda chooni sakata limeishia, Maisha yanaendelea kwa kuhitaji chakula kingine.
Huu ni muda sahihi, muda wa kuacha, nyuki hakumbatiwi wala miba haitafunwi.
Utambue huu muda.
Muda wa kuachana ni muhimu hasa ukifikia, Ni muhimu kuujua na kuutendea haki.
Kuendelea kumkumbatia mtu aliyekuchoka ni hatari matokeo yake ni vifo na ukatili, mume kamuua mke au mke kumchoma moto mume.
Zamani ulikuwa thamani Sasa wa kazi gani, usijipe jaka rohoni, muepuke shetani.
Nenda anakusubiri, yule mwengine wa kweli, penzi lenye shubiri ni dhambi kulivumili.
Kwani yeye ni nani mpaka usimuache achana na hayawani siku za kuishi ni chache.
Hajabandua kiungo kisafishe ukihifadhi mwenye matumizi nacho akikute kipo safi.
Usivumilie karaha zisizo na marekebisho, Leo kosa kesho kosa,hapa kosa kule kosa, makosa ya makusudi.
Makosa mfululizo Usaliti na Dharau, Kiburi na ushubwada amua kutupa Kule, muache aende zake.
Thamani yako adimu hayuko nayo mwengine usiruhusu dhalimu akaitupa kwengine, Furaha yako muhimu anaijua mwengine, achana nae wazimu moyo wako upone.
Nakusihi umuache usingoje akuache yeye, muoneshe nguvu yako abaki ajute yeye.
Utampata mwengine mkarimu na mwenye upeo, mpole na mnyenyekevu aliyeumbwa kwa ajili yako.
Tena mwenye taaluma, na hodari wa mapenzi, mwenye moyo wa kuchuma na bingwa wa kuenzi.
Heshimu muda ndugu yangu, usisubiri matokeo mabaya ukaweka historia mbaya, ukayatenda mabaya ya jinai na aibu.
Muache aende kwa amani ya bwana.
Leo nipo hapa kukusihi Usihuzunike bali usheherekee ukiziona dalili za siku.
Siku ya kuachana...
Kama umevutiwa na Andiko hilo Unaweza kulisikiliza na kulidownload pia kwa njia ya Sauti kwa kuBofya Link hii hapa https://youtu.be/rz6fJhfpirk