NIMEZAMA TOPENI

uvundo nausikia, karaha tupu puani.
tope hili madhara, afya yangu hatiani.
sinayo hamu yakula njaa ingali tumboni.
ninani wakunitoa nimezama topeni!

siwezi kujinasua tope limeniganda
nashindwa kujiondoa,kihoro kimenipanda.
masaa yanasogea joto lazidi kupanda
tope lanizidia mwili wote waganda

tope hili maajabu launguza mwili wangu
nimepuuza ya babu na sasa majuto yangu
ubishi ndio sababu wahaya mateso yangu,
nani sasa wakutibu matope mwilini mwangu.

sina wakumlaumu kadhia mejitakia
tope hili lasumu nimezama kwa umbea!
sinayo tena hamu, mecheza pata potea
meupata ugumu kwa nnayojionea

ombea yasikupate,utageuka msongo.
niliambiwa ningoje nikaona ni porojo,
nikauvaa mtope sasa wanipa kipigo
zamishwa mwili wote iliyobaki ni shingo


tope flani karaha, kulijua ni vibaya
limejua kunihadaa bila soni wala haya
chini yake nimekaa, siwezi tena kimbia
maumivu majeraha nafsi yangu yajutia

mwanzo niliona tamu kuchezea tope hili,
 lilinikidhi na hamu, sikuiona shubiri,
ghafla likabadilika,
tamu ikawa chungu
likanifika gharika,
saidia Mungu wangu!

Hili tope mauti mezama mebaki kichwa,
zimeisha tashtiti, kama jua lishapatwa
 najuta kula yamini nakuzama ndani yake,
nionayo siyaamini kiburi chote nichake!

viganja vi hatarini vimekamata makali,
vimeuacha mpini tope limekua kali
naanzaje kukinzana maumivu yanatosha!
siwezi kupambana tope lishaniangusha

hili tope ni laghai linatumia uchawi,
limbwata kwenye chai, mie hapa sielewi
urembo na tabasamu hugeuka tafrani,
mwanzowe ni kama utani.
mwishowe ni ndita kweli,
shubiri yatapakaa nyongo yachanganyika
 maisha hua balaa, niyaonayo najuta.

kilio cha kifo changu kitokanacho na tope
chafanana na wenzangu waliopo pande zote,
sijazama peke yangu kwenye hizi hila za tope.
Mtukufu mola wangu nifanye humu nitoke!
hili tope nilaana lipige liniepuke.

afya yangu ni tanzia maana sili nikashiba,
 nazorota mwili wangu marafiki wanacheka
wanahoji sifa zangu ni wapi zilipogota,
zipo wapi mbwembwe zangu zaishi matopeni!

tope wewe tope wewe sikudhani nihasidi!

mwanzoni haukuwa tope ulikuja umbile maji,
ulisema naweza oga, nikunywe nikijisikia, ukajiita maji ya afya nikauona Uhai! nikazipiga na chafya kumbe ulinilaghai na sasa umekuwa tope wanizamisha ndani!!! tope wewe tope wewe MUNGU wako anakuona.

hakika tabia zako tope wewe zachefua
upole ndio sifa yako ulipoanza kunijia
hizi hasira zako niwapi zimetokea
punguza  hila zako mwenzio sijazoea

Tope gani kisirani huruma hauko nayo
umenifika shingoni
basi badilisha moyo
nipatie ahueni
nishakiri upoyoyo
tamaa sitotamani
siyo sitasema ndiyo.

jamani nani ajua siri ya hili tope
aje kuniambia ntamlipa chochote
mwenzenu litaniua
kwa mateso ya upweke
mechoka kukumbatia uchungu wa adha zake.

ASANTENI KWA HISTORIA

"Zaidi ya miaka 50 tangu kufanyike mapinduzi matakatifu visiwani zanzibar, mapinduzi ambayo yamewaweka huru ndugu zetu visiwani humo, hakika historia ya zanzibar imejiandika vema kupitia wana mapinduzi wakiongozwa na Sheikh Abeid Aman Karume na wengine wengi kama vile Okelo na wengineo..leo naifurahia historia ya zanzibar na nawashukuru wanamapinduzi kwa kutuachia historia hii yenye funzo kubwa kwetu, funzo la uzalendo na ujasiri .

Na
Omar Zongo 

Historia ilotukuka, historia ya heshima, historia isofutika, asanteni kwa historia.

Meshika kitabu changu aliniachia babu, kitabu cha mapinduzi kina nyingi historia.

Kitabu chanikumbusha niishi kwa uzalendo, maovu kuyaondosha nisimamie upendo, upendo wa watu wangu, upendo wa nchi yangu, upendo kwa taifa langu.
Asanteni kwa historia.

Historia yanifunza nisiishi kiunyonge mgeni nisomuelewa nimfukuze aende.

Historia hii tamu, nzuri tena adimu, historia  adhimu, yanipenya kwenye damu.

Historia yasema wenyeji walisimama, haki wakaiandama kuipata himahima, wageni wenye hila msimamo wakauona, dhamira ikawasuta pindu wakapinduka..

Mabio wakayatoa, visigino visogoni, hofu ikawatawala wakarejea makwao.

Historia yasema imeshajiandika hakuna wakuifuta okelo yamkumbuka.

Karume simba imara historia yamtaja yasema yeye ni bora mja mwenye tija.

Mwanzoni tu mwa mwaka, tisa na sitini Na nne tarehe 12 Na mbili historia yakariri.

Historia yataja wageni wale watesi hakika wanayo kesi kwa hila zao dhalili.

Walifilisi wenyeji wakajichotea Mali, wakajikabidhi mji watawala ndio wao.

Wakabagua wenyeji kisa rangi tofauti, wakatafuta ulaji kwa jasho la babu zetu.

Ardhi yenye rutuba wakatangaza niyao, mito milima bahari vyote vikawa vyakwao.

Wakamiliki warembo wenyeji wenye maumbo, wazuri wenye uturi wakasema Mali yao.

Dada zao sumu kwetu, wakwetu halali yao, wenyeji wale si watu historia yanijuza.

Historia yataja tangu mipango kuanza, wenyeji walipochoshwa mapinduzi wakaunda.

Yasema nikama muvi, luningani twaziona, mabunduki ya kijeshi wazo lilishawazuka.

Sultani tupa kule jamsheed mwanakharamu, Na wenzake wote chali Uhuru shika hatamu.

Hongera historia u
mepangwa ukapangika, sasa napata kujua niwapi nilipotoka.

NIMEPATA PESA

Na.
BinZongo

Shida shida sasa basi tayari ninazo pesa! Pesa nyingi za kuzidi sio zile za mawazo.

Nabadilisha mavazi, chakula nikipendacho, magari ya kila rangi kampuni tofauti.

Jumba langu ni 'palace' mtawala ndio mie
Limezingirwa Na fensi, himaya kubwa ijue.

Ulinzi imara sana, majambazi halahala! Mabaya mtayavuna mkija kifalafala.

Niite bosi, tajiri we mwenyewe siunaona! Yajana siyakumbuki usije yataja tena.

Dhiki ndio kitu gani! Habari zakizamani ukinitajia tena shtaka mahakamani.

Kwasasa pesa ninayo mpenzi naomba nielewe maamuzi yafuatayo naomba uyatambue

Nahisi haunifai, kuishi nawe aibu, japo tumetoka mbali ila sasa Tabutabu.

Siwezi tumia nawe pesa hizi pomoni, nataka mtu mwengine nimuingize moyoni

Sema nikupe nini ili tuachane leo, tusahau yazamani sasa nimepanda cheo.

Umasikini enzi zetu utajiri zama nyengine.
Pesa sasa zanitosha kumtafuta mwengine.

Ongeza basi mvinyo tuendelee kuongea, hivi sasa nina meno natafuna hili penzi.

Tafuta aina yako mimi sasa siyo tena, mipesa yangu lukuki shimo langu limetema.

Nyie watu nikomeni eti nimebadilika, mambo yangu yaacheni naishi ninavyotaka.

Sitaki kukaa dar, Paris napatamani, marekani sitakaa Kim hataki amani.

Mswahili kama wewe mambo yako yakijadi, mzungu ndio nioe nataka nikupe kadi.

Kusanya mabegi yako nikupe Na fungu lako kaishi maisha yako sikuhitaji mwenzako...


"Don't expect!!! Maisha hayabadiliki ila watu ndio hubadilika..."